Warembo wa Miss Tanzania na Kazi za Jamii.

0
1399

219Na: Hidan Ricco.
Baada ya mashindano ya urembo ya Miss Tanzania kusitishwa kwa muda hapo Desemba 2014 yalifunguliwa tena mapema mwezi Julai 2015 baada ya waandaaji wake Kampuni ya Lino International Agency Limited kutimiza masharti waliyopewa na Baraza la Sanaa la Taifa. Basata.

Pamoja na kufanya mabadiliko katika safu ya wajumbe wa Kamati ya Miss Tanzania, kamati ambayo ndiyo inasimamia na kuratibu mashindano hayo. Kamati hiyo pia imekuja na mapendekezo na ushauri kwa uongozi wa Kampuni ya Lino International Agency kuwaandaa mapema washiriki wanaoshiriki mashindano ya urembo ya Miss Tanzania katika mashindano madogo ndani ya shindano kubwa la kumtafuta mrembo wa Dunia yaani Miss World.
Katika fainali za shindano la kumtafuta mrembo wa Dunia yapo mataji madogo ambayo hushindaniwa na washiriki wote.
Mataji hayo ni.
1. Mrembo na Malengo. (Beauty with Purpose)
2. Mrembo mwenye kipaji. (Miss Talent)
3. Mrembo anayevutia katika picha. (Miss Photogenic)
4. Mrembo mwanamichezo. (Top Sport Woman)
5. Mrembo Mwanamitindo. (Top Model)

Washindi watano wa mataji hayo hupata tiketi ya kuingia katika hatua ya pili ya kumi bora (Top 10) na mrembo atakayefanya vizuri zaidi huingia katika hatua ya 3 ya Tano Bora (Top 5) na hatimaye kutangazwa mshindi wa Fainali hizo.

Warembo wa Tanzania walioshiriki Fainali za mrembo wa Dunia tangu mashindano ya Miss Tanzania yaanzishwe mwaka 1994, ni mrembo Nancy Sumari Miss Tanzania 2005, ambaye aliweza kuwakilisha vema nchi yetu pale aliposhinda katika shindano dogo la Mrembo Mwanamichezo, na hatimaye kushinda Taji la Mrembo Bora wa Africa
(Miss World Afirca 2005). Taji lililompa nafasi ya kuingia katika hatua ya mwisho ya Fainal yaani Top 5.

Mrembo Nancy Sumari atakumbukwa daima katika historia ya Tasnia ya urembo nchini, kuwa ni mrembo wa kwanza kupata zawadi ya juu katika mashindano ya urembo ya Miss Tanzania. Pamoja na kupewa zawadi ya pesa taslimu mrembo huyu alipewa zawadi ya gari, pamoja na nyumba aliyokabidhiwa eneo la Tabata Barakuda.

Baada ya hapo Kamati ya Miss Tanzania pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Lino International Agency iliweka mikakati ya kuwanoa warembo wake kushiriki na kushindana katika mataji haya madogo ili kuweza kuiletea sifa nchi yetu.

Mwaka 2012 Miss Tanzania Brigitte Alfred aliweza kuibuka kidedea katika shindano dogo la mrembo wa Dunia pale aliposhika nafasi ya 3 katika shindano la Mrembo na Malengo, (Beauty with Purpose). Miss Tanzania 2012 Brigitte Alfred ameweza kujenga bweni la kusaidia kuwatunza watoto wanaoishi katika mazingira magumu, watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albino) huko Buhangija Shinyanga.

Ujenzi wa bweni hilo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 60 ambazo mrembo huyu kwa juhudi zake akishirikiana na Uongozi wa Kamati ya Miss Tanzania aliweza kuchangisha pesa hizo na kufanikisha ujenzi wake, mbali na hivyo Mrembo Brigitte Alfred amekuwa Balozi mzuri wa watoto wenye ulemavu wa Ngozi Albino akiwasaidia na kuwatetea kwa kila hali.

Itakumbukwa kwamba jamii hii ya walemavu wa ngozi Albino hususan watoto wadogo wamekuwa wakiuwawa sana kutokana na imani potovu za ushirikina. Mkanda wa video uliorekodi matukio kadhaa ya walemavu hawa pamoja na usaidizi uliotolewa na Miss Tanzania huyu Brigitte Alfred ndio iliyosababisha ashinde nafasi ya 3 katika shindano dogo la Fainali za shindano la urembo la Dunia kwa mwaka 2012.

Baada ya kuwashwa kwa moto huo mwaka 2012 mrembo aliyefuata Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa aliuendeleza moto huo kwa kushiriki katika shindano dogo la Mrembo wenye mvuto Miss Personality pale alipata kura nyingi kutoka mabara yote ya dunia na kumuwezesha kushika nafasi ya 3 Katika shindano hilo.

Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa pamoja na urembo wake alionao pia aliwasilisha video ya kazi za jamii zinazoonyesha akifundisha watoto wadogo na vijana somo la hesabu katika shule mbalimbali hapa nchini. Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa ni bingwa wa somo la Hisabati ambaye alishindanishwa na wanafunzi wengine wa kidato cha 6 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mss Tanzania 2014 Lilian Kamazima mrembo anayeshikilia taji kwa hivi sasa nae pia amewakilisha nchi yetu vema katika mashindano ya urembo ya dunia mwaka 2015 katika shindano dogo la Mrembo na Malengo (Beauty with Purpose) pale alipoingia katika Kumi Bora (Top 10) ya shindano hilo.

Mrembo Lilian Kamazima aliwasilisha video ya kazi za jamii alizozifanya kusaidia akina mama na wasichana wenye matatizo ya Fistula. Miss Tanzania 2014 Lilian Kamazima pia ni Balozi wa Hospital ya CCBRT inayotoa matibabu kwa waathirika wa ugonjwa huyo.
Warembo wa Miss Tanzania na kazi za jamii ni kauli mbiu ambayo imekuwa ikitekelezwa mwaka hadi mwaka sio tu kwa warembo wa Taifa walioshinda nafasi ya Miss Tanzania bali pia kwa warembo wa Mikoa, Wilaya na Vitongoji.
Mrembo wa Milenea Miss Tanzania 1999 Hoyce Temu ni mrembo anayeendeleza kauli mbiu hiyo kwa kuendelea kufanya kazi za jamii mwaka hadi mwaka na kuhamasisha warembo wengine kuiga mfano huo.

Warembo wengi waliopitia Mashindano ya urembo ya Miss Tanzania wamekuwa wakiendeleza kauli mbiu ya Mrembo na Malengo pale walipoanzisha Taasisi mbalimbali za kusaidia jamii wasiojiweza na wale wanaoishi katika mazingira magumu. Baadhi ya warembo hao ni pamoja na Miss Tanzania 2001 Happiness Magese, Miss Tanzania 2008 Nasreen Karim. Miss Tanzania 2012 Brigitte Alfred. Doris Molles Miss Tanzania 2014 mshindi wa 3, na wengine wengi.

Jumatatu wiki Miss Tanzania 1998 Basila Mwanukuzi alizindua Taasisi yake ya Basila Mwanukuzi Foundation yenye lengo la kusaidia akina mama wajasilia mali maarufu kama Mama Lishe.

Taasisi ya Basila Mwanukuzi itajikita zaidi katika kusaidia wanawake wa makundi tofauti kujitoa kutoka kwenye hali ya kusaidiwa hadi kuweza kusimamia miradi yao wenyewe na hivyo kubadili hali zao za maisha na kiuchumi.
Kama sehemu ya uzinduzi wa Taasisi hiyo ya Basila Mwanukuzi imezindua mradi wa Wezesha Mama Lishe Tanzania, ukiwa na lengo la kuwawezesha mama lishe kwa kuwapatia elimu ya ujasiliamali, afya pamoja na kupika chakula bora chenye kuzingatia virutubisho na uwezeshaji wa kupata mikopo na kuongeza mitaji yao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Mwanzilishi wa Taasisi hiyo Miss Tanzania 1998 Basila Mwanukuzi alisema taasisi yake iliguswa na changamoto nyingi zinazolikabili kundi hili la mama lishe kwa kipindi kirefu bila ya msaada wowote.

Baada ya kufanya utafiti kwa muda mrefu na kuzungumza na mama lishe tumegundua kina mama hawa katika mazingira yao tofauti ya kazi wana changamoto zinazo fanana kama mazingira mabovu ya kazi na ukosefu wa mitaji, hivyo basi mradi huu utajikita katika kusaidia kina mama lishe watambulike, waweze kujiamini na kupewa thamani katika jamii. Alisema Miss Tanzania 1998 Basila.

Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Tanzania, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye ndio alikuwa Mgeni wa Heshima katika hafla hiyo alisema kwamba nusu ya nguvu kazi ya taifa inalishwa na kina mama hawa, hivyo kuna haja kubwa kabisa kuwasaidia akina mama hawa na kurasimisha mradi huu, kwani ni njia mojawapo ya kusaidia kuwainua kiuchumi, na pia wanachangia katika kuongeza pato la taifa kwa kulipa kodi, lakini pia vyakula vya mama lishe ni tegemeo la watanzania wengi kwani bei yake huwa ni nafuu. Aliwesema Waziri Ummy.

Utekelezaji wa Mradi wa Wezesha Mama Lishe utajumuisha uundaji wa vikundi vya ushirikiano wa mama lishe ili kubadilishana uzoefu na pia uanzishaji wa shughuli za kujiingizia kipato kwa Mama Lishe na utafutaji wa zabuni za kuandaa vyakula vya harusi na kadhalika.

Mpaka sasa mradi wa Wezesha Mama Lishe umefanikiwa kuanza kuwaandikisha mama lishe waliopo jijini D’salaam na baadhi wameanza kupata mikopo ya riba nafuu, huku ukitaraji kupanuka nchi nzima ili kuwafikia akina mama lishe wengi zaidi.

Hii ndio maana halisi ya Mrembo na Malengo, na napenda kuona warembo wengi wa Miss Tanzania wakiendeleza falsafa hii na kwamba Wizara yangu itakuwa pamoja na nyinyi katika kusaidia jamii na kuwaendeleza pia. Alisema Waziri Ummy Mwalimu huku akitoa sifa nyingi na pongezi kwa uongozi wa Kamati ya Miss Tanzania.

Ni matarajio yetu kwamba warembo na washiriki wa mashindano ya Miss Tanzania wataendeleza kauli mbiu hii ya Mrembo na Malengo, kwa madhumuni ya kusaidia jamii na wananchi wa Tanzania kwa ujumla.

Picha zote na: Hidan Ricco.

NO COMMENTS