Walioibia Bandari “mamilionea”

0
824

Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), wengi wao wakiwa ni watoto wa vigogo, wamekuwa mamilionea kutokana na wizi wa fedha za tozo za bandari ambao imeelezwa kuwa wamekuwa wakiufanya kwa miaka mingi.

Mtoa taarifa wetu ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliliambia Nipashe jana kuwa serikali imeibua sakata hilo ikiwa imechelewa kwani wengi wa wafanyakazi hao walishakuwa matajiri wa kupindukia, wakimiliki vitega uchumi mbalimbali na magari ya kifahari.

Alisema wizi uliofanywa na wafanyakazi hao wakishirikiana na benki moja ya biashara ni kufuru kwani ulifanyika mchana kweupe kwa kutoa risiti ambazo baada ya fagia fagia iliyoanzishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, zimeonekana hazitambuliwi na TPA.

Majaliwa aligundua upotevu wa makontena zaidi ya 11,000 ambayo hayakulipiwa ushuru bandarini (Wharfage charges) mwishoni mwa mwaka jana.

“Kukamatwa kwa mtoto wa Kova, Masoud ni sawa na tone la maji baharini, wako watoto wengi wa vigogo ambao hawajakamatwa na ndiyo sababu hadi leo suala la kauwafikisha mahakamani linakuwa la kusua sua,” alisema mtoa habari wetu huku akionyesha nyaraka mbalimbali.Kusoma zaiid bofya

“Watu pale bandarini wanaajiriwa kwa vimemo na ndiyo sababu walipata hata ujasiri wa kuchukua mamilioni ya fedha za TPA.”

Kwenye sakata hilo serikali imeeleza kupoteza zaidi ya Sh. bilioni 47 ambazo zimeingia kwenye mifuko ya watumishi hao.

Alitaja eneo lingine lililowatajirisha wafanyakazi hao wa bandari kuwa ni meli za mafuta zinazokuja kupakua mafuta katika bandari ya Dar es Salaam kwani asilimia kubwa ya tozo ambazo meli hizo zinapaswa kuilipa TPA imekuwa ikiishia kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

“Ndugu yangu serikali ikitaka kuwafunga watu itengeneze magereza ya kutosha maana watu wamekula mpaka wamesaza,” alisema.

“Hebu fikiria mameli makubwa yanayoleta mafuta kila siku yanapaswa kulipa TPA shilingi ngapi? Sasa malipo mengi hayafiki sehemu husika maana kuna namna wanagushi kisha wanagawana na ni kikundi cha watu hao hao.”

Aidha, alisema wafanyakazi hao wamekuwa na utajiri wa kutisha kwani nyaraka zilizoghushiwa kwa miaka yote bandarini hapo, zikikusanywa na kuhakikiwa ni mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kusaidia kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.

Mtoa taarifa huyo alimwonyesha mwandishi wa habari hizi orodha ya risiti feki zilizotolewa na watumishi hao wa bandari, ambao wengine wanaendelea kuisadia polisi kutokana na wizi huo ambao umeelezwa kuwa uligeuka kuwa mchezo wa kawaida.

Moja ya risiti ya malipo ya Sh.7,700,294 zilizotolewa na moja ya makampuni ya wakala wa forodha iliyopitishwa na mtumishi wa Mamlaka hiyo, Charles Nambole, inaonyesha kuwa na mihuri mbalimbali ya TPA lakini baada ya mtikisiko uliosababishwa na Waziri Mkuu bandarini hapo, ilihakikiwa na kuelezwa kuwa ilighushiwa.

Risiti hiyo iliyotolewa Septemba 23, 2014 ambayo ni miongoni mwa mamia ya risiti zilizotolewa na wafanyakazi wa TPA, ilifanyiwa uhakiki Jumatano iliyopita na kuandikwa kuwa haionekani kwenye mifumo ya kompyuta za mamlaka hiyo, “Invoice in the system is cancelled”.

“Hivi risiti kama hii ambayo umepewa na mamlaka husika na ukaruhusiwa na bandari kavu kuondoa mzigo wako utaota kwamba imeghushiwa?

“Lakini cha kushangaza siku hizi TPA imeanza kamata kamata ya wakala wa forodha wenye risiti za aina hii badala ya kuwakamata wafanyakazi waliotoa risiti hizo.

“Kuna taarifa kwamba wameshakamata baadhi lakini wengi bado,” alisema mtoa taarifa wetu.

Risiti nyingine ambayo Nipashe ina nakala yake, inaonyesha kusainiwa na ofisa mwingine wa TPA, Bonasweetbeth Kimaina, kwa malipo ya Sh.2,469,253, kama tozo ya bandari iliyotolewa kwa moja ya makampuni ya wakala wa forodha lakini nayo ilipohakikiwa ilionekana kuwa ilighushiwa.

Risiti hiyo yenye mihuri na taarifa mbalimbali ya TPA iliyohakikiwa Januari 13 pia iliandikwa juu yake kwamba ni ya kughushi na haikubaliki ingawa ilipitishwa na ofisa wa mamlaka hiyo ambaye mtoa taarifa alisema kuwa tayari alishakamatwa na polisi.

“Wakala wa forodha wamekuwa wakilipa malipo ya tozo miaka yote na wamekuwa wakipewa risiti za namna hii, sasa fikiria wizi huo umefanyika kwa zaidi ya miaka 10; hawa watu watakuwa na utajiri wa namna gani?
“Mkuu wa Usalama wa TPA alishawahi kuandika ripoti ya madudu yote haya lakini alipuuzwa.”

Katika mgogoro huo, kampuni 283 za wakala wa forodha zinadaiwa kupitisha kontena zaidi ya 11,000 pamoja na magari zaidi ya 2,000 bila kulipa wharfage Charges.

Mamlaka ya Bandari (TPA), ilishakamata watumishi wake 15 ambao wanadaiwa kuhusika na ukusanyaji wa tozo hizo ambao wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 47, kwa kutoa makontena hayo katika bandari kavu ICDs.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

NO COMMENTS