Trump azungumzia video ya al-Shabab.

0
708

Trump
Mgombea wa urais Marekani Donald Trump kwa mara nyingine ametetea pendekezo lake la kutaka Waislamu wazuiwe kuingia Marekani baada ya wito huo kutumiwa na wapiganaji wa al-Shabab kwenye kanda ya video ya kutafuta wafuasi.
Bw.Trump, anayeongoza miongoni mwa wanaotafuta tiketi ya chama cha Republican, amesema watu wamemsifu kwa kuwa na ujasiri wa kuangazia jambo hilo “ambalo wengine wameamua kupuuza”.
Al-Shabaab walitumia maneno hayo ya Trump kwenye video ya propaganda ya kutafuta wafuasi wakisema ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi na chuki dhidi ya Waislamu vimesheheni Marekani.
“Sasa watu wanaanza kuzungumzia hili,” ameambia kituo cha runinga cha CBS News.
Kundi hilo liliweka sehemu ya kanda ya video ya Trump akikariri wito wake wakati wa mkutano wa kampeni kwenye video yao ya propaganda ya karibu saa nzima.
Katika mahojiano na watangazaji wa kipindi cha Face the Nation cha CBS News, ambacho kitapeperushwa baadaye Jumapili, Bw Trump aliulizwa kuhusu jinsi al-Shabab wanatumia matamshi yake kutafuta wafuasi.
Chanzo:BBC

NO COMMENTS