Taifa Stars yagonga Mwamba!

0
665

Taifa stars hoi.
Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imegonga mwamba mwingine hii Jumamosi baada ya kuangushwa kwa bao 1-0 na timu ya Taifa ya Morocco Simba wa Atlas kwenye uwanja wa Taifa Daressalaam Tanzania.

Bao hilo lilifungwa dakika mbili kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika limeipa ushindi Morocco ambapo mpaka mapumziko tayari Tanzania ilikuwa imeshalala 1-0. Dan Mrwanda wa Tanzania atajilaumu mwenyewe kwa kukosa nafasi ya wazi kunako dakika za mwanzo za mchezo huo.

Kipindi cha pili Tanzania ilitumia muda mwingi kuokoa mashambulizi hatari ya Morocco langoni mwao mbele ya uwanja uliojaa mashabiki wakiongozwa na mgombea urais kwa tiketi ya CCM na Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

Tanzania pia ilipoteza nafasi kadhaa za kufunga kwa mujibu wa gazeti la Daily News wachezaji wa kimataifa wa Tanzania Henry Joseph anayecheza soka ya kulipwa Vietnam na Nizar Khalfan wa Vancouver White caps ya Canada walifanya jitihada kadhaa lakini wafungaji wa kutegemewa Mrisho Ngassa na Danny Mrwanda walishindwa kumalizia kupata magoli.

Dakika za mwishoni mwa mchezo Tanzania iliongeza mashambulizi lakini ukuta wa Simba wa Atlas uliweza kudhibiti mashambulizi hayo.

Taifa stars sasa ina pointi moja tu kwenye kundi D ambalo sasa Morocco wamejiweka kwenye nafasi nzuri wakiwa juu na pointi 4. Algeria watacheza Jumapili ijayo na Jamhuri ya Afrika ya kati kujaribu kurudisha heshima yao wakati Afrika ya kati walioishikilia Morocco kwao na suluhu bila kufungana watakuwa wakifanya juu chini kuendeleza hilo.

Katika michuano hiyo pia kwenye kundi E Cameroon ilijikuta ikibanwa na Congo nyumbani kwao na kutoka suluhu ya bao 1-1. Hivi sasa Cameroon wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi 4.

Na katika kundi K Malawi iliichabanga Chad 6-2 na kushika nafasi ya pili kwenye kundi hilo nyuma ya Bostwana inayoongoza kundi hilo na pointi 10.

NO COMMENTS