RC: Mvua imeivuruga D’Salaam.

0
352

IMG-20150507-WA0195Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amesema mvua zinazoendelea kunyesha, zimelivuruga jiji na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, huku watu wanane wakipoteza maisha. Sadiki aliyasema hayo jana ofisini kwake muda mfupi baada ya kumalizika kikao cha kutathmini mafuriko hayo kilichohusisha wakuu wa wilaya za mkoa huo, Ilala, Kinondoni na Temeke.

Pia, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na maofisa wa Kitengo cha Maafa mkoa.

Sadiki aliliambia gazeti hili kuwa jiji haliko kwenye hali nzuri kwani barabara zaidi ya 20 zimeharibiwa, madaraja kadhaa, makaravati yamesombwa na maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika baadhi ya maeneo.

Kutokana na hali hiyo aliwasihi wakazi wa Dar es Salaam kuwa wavumilivu hadi mvua hizo zitakapopungua na kuruhusu ujenzi kufanyika.

“Nimewaagiza viongozi wa manispaa kufanya kila linalowezekana kurudisha mawasiliano katika maeneo ambayo madaraja yamevunjika ili shughuli ziendelee kama kawaida huku tukijipanga kwa ajili ya kurekebisha maeneo mengine yaliyoathiriwa.”
IMG-20150507-WA0201

Sadiki aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua hizo ni pamoja na Keko, Chang’ombe Maduka Mawili, Yombo Vituka, Vingunguti, Africana, Msasani Bonde la Mpunga, Jangwani, Manzese, Kigogo, Mburahati, Boko na Basihaya.

Kwa mujibu wa Sadiki barabara 18 za Wilaya ya Kinondoni zimeharibika kwa viwango tofauti hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji na wakati mwingine kuleta msongamano.

“Barabara nyingi zimeharibika ingawa Wilaya ya Kinondoni imeonekana kuathirika zaidi, lakini tumeruhusu ziendelee kutumika kupunguza msongamano, ila tutazifunga tena endapo mvua zitaendelea kunyesha ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza, endapo zitatumika zikiwa zimefurika maji.”

Miongoni mwa madaraja yaliyoharibika ni Mwanamtoti linalounganisha Mbagala na Mtoni Kijichi, Kinyerezi ambalo halipitiki kabisa baada ya kusombwa na maji.
IMG-20150507-WA0205

Shule kufungwa

Licha ya kukiri kuwa mvua hizo zimesababisha mahudhurio hafifu katika shule za msingi, Sadiki alisema kwa sasa hakuna mpango wa kufunga shule hizo, isipokuwa zile zilizopo kwenye mazingira hatarishi.

“Tumefunga kwa muda shule ya Msingi Vingunguti baada ya kuona imezingirwa na maji, hata hao wanafunzi wasingeweza kusoma, lakini maeneo mengine masomo yanaendelea kama kawaida ingawa hali ya maudhurio inaonekana siYo nzuri kutokana na hali ya hewa,” alisema.

sack Mtakimwa ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Mbagala Kuu, alieleza kuwa wanalazimika kuwaruhusu wanafunzi kurudi nyumbani mapema kwa kuhofia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

“Mahudhurio yamepungua sana na wapo watoto wanaochelewa kufika shuleni, hatuwezi kuwarudisha wala kuwaadhibu kwa vile tunalewa hali halisi,” alisema Mtakimwa.

Hali hiyo pia ilionekana katika Shule ya Msingi Maendeleo ambayo ina wanafunzi 3,068, lakini nusu ya wanafunzi wanashindwa kuhudhuhuria masomo katika kipindi hiki cha mvua.

Waathirika ‘imekula kwao’

Kuhusiana na waathirika wa mafuriko hayo, Sadiki alisisitiza kwa kusema hakuna namna ambayo Serikali itawasaidia, kwa kuwa waliambiwa kuhama kwenye mazingira hatarishi kwa muda mrefu.

“Walishaambiwa muda mrefu wahame hawataki tena kwa bahati nzuri siku hizi Mamlaka ya Hali ya Hewa wanatoa taarifa mapema, lakini wakaendelea kung’ang’ania sasa kama mtu hataki na hili limemkuta itabidi ajitegemee.

“Mpaka sasa hatuna msaada wa aina yoyote, kama itatokea watu wakajitolea kuwasaidia tutashukuru sana,” alisema Sadiki.

Jangwani

Baada ya nyumba za wakazi wa maeneo ya Magomeni Mapipa, Mikumi na Bonde la Mkwajuni kuzingirwa na maji, baadhi yao wamehamia kwenye kituo cha mabasi yaendayo kasi (DART).

Gazeti la Mwananchi lilipita kushuhudia hali halisi katika maeneo mengi ambayo yaliyozingirwa na maji kuanzia juzi usiku, na kukuta maeneo machache yakiwa yamepungua maji huku mengine yakiwa bado yamezingirwa.

Lilishuhudia pia wakazi wa maeneo ya jirani na Jangwani wakiwa wameweka makazi katika kituo hicho kilichopo hatua chache kutoka katika daraja la Kajima, ambalo hapo jana lilisababisha barabara ya Morogoro kufungwa kwa muda kutokana na maji kupita juu ya daraja hilo kwa kasi, wakiwa wameweka makazi kituoni hapo.

Wakazi hao wakiwa na vifaa vyao ikiwamo mabegi ya nguo, magodoro, na mizigo mbalimbali, huku baadhi ya nguo zikionekana kuanikwa katika mabomba ya chuma yaliyopo kituoni hapo kuashiria kuwa wamefika.Kusoma zaidi bofya

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya watu hao walisema kuwa hawahitaji mahojiano, na wapo hapo kwa muda mvua ikikatika watarudi katika maeneo yao.

“Hatutaki kupigiwa kelele, tupo hapa kwa muda, msije kuona kama mmepata sehemu ya kupata habari, haya ni matatizo kila mtu yanampata, yakiisha tunarudi katikia maeneo yetu, ”alisema mmojawao aliyejitambulisha kwa jina la Saidi.

Daraja la eneo hilo ambalo juzi lililokuwa limefungwa kwa muda lilifunguliwa asubuhi na lilianza kutumika.

Magomeni Sunna miili yaopolewa

Licha ya kupigiwa kelele ya kutakiwa kuondoka eneo hilo, wakazi wa Mtaa wa Sunna Magomeni wameonekana wakihama baada ya maji kuja kupitia kiasi tangu juzi.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa eneo wa Serikali ya Mtaa huo Mgaya Mgaya, alisema kuwa zaidi ya familia 78, hazina makazi kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji.

Mgaya ambaye alikutwa eneo la tukio ikiwamo na nyumba yake kujaa maji alisema kuwa Mtaa huo una wakazi zaidi ya 4,000, miongoni mwao ni hizo familia 78, ambazo hazina makazi huku baadhi yao zikiwa zimeomba hifadhi kwa jamaa zao.

“Hivi sasa ninaorodhesha majina ili kuangalia namna tutakavyosaidiana ikiwamo watu wanaohitaji kutusaidia wawe na idadi kamili, ”alisema Mgaya.

Mgaya aliongeza kuwa katika eneo la Mto Ngo’mbe iliokotwa miili miwili ya watu wakiwa wamefariki dunia, mmoja ukibainika kuwa ulisombwa na maji eneo la Tandale na kuokotwa katika eneo hilo.

Katika maeneo ya Kigogo, Tandale, Mikocheni licha ya kujaa maji ilionekana maji yamepungua licha ya kuwapo msongamano wa magari katika barabara nyingi.

Mmoja aopolewa Magomeni Mkwajuni
Baadhi ya wakazi wa eneo la Kinondoni Mkwajuni waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa asubuhi ya jana kuliopolewa mwili wa mwanaume mmoja.

Godfrey Peter mkazi wa eneo hilo alisema kuwa waliokota mwili huo saa moja asubuhi ukielea kwenye maji, huku baadhi ya mashuhuda wakisema wanamfahamu na kueleza kuwa anaishi eneo hilo la Mkwajuni.

“Inaonekana alisombwa na maji eneo lingine huko juu, kwani kuna watu walikuwapo wakati anaokolewa walisema kuwa wanamtambua anaishi Mkwajuni hii, ”alisema Peter baada ya juhudi za kumpata Mjumbe wa eneo hilo kugonga mwamba kwa madai kuwa na yeye nyumba yake imeingia maji.

Goba, Mbezi yagawanyika

Kutokana na mvua hizo kuendelea wakazi wa maeneo ya Goba, Mbezi hawana mawasiliano kutokana barabara inayounganisha maeneo hayo kuharibika vibaya.

Wakazi wa eneo hilo ambao walikuwa wakitumia njia hiyo kwa usafiri kutoka Mbezi ya Kimara kwenda Goba, lakini yamelazimika kuacha kufanya safari za njia hiyo, hivyo kuwalazimu kutembea kwa miguu.

Abdallah Abdu alisema kuwa tangu juzi, daladala zimeacha kupita eneo hilo kutokana na barabara hiyo kuwa mbaya, kutokana na matengenezo yaliyoanza tangu mwaka jana kutokamilika.

“Hapa usumbufu ni mkubwa hasa kwa wakazi wa Goba, kwa sababu njia hii ilikuwa ndiyo fupi, lakini sasa ili kupita lazima uogelee tope hili, ilivyochimbika haipiti pikipiki, bajaji sikuambii gari, lazima linase, ” alisema Abdu.

Polisi wathibitisha kutokea kwa vifo hivyo

Kamanda wa Polisi Kanda ya Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo vilivyotokea kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Kova alisema kuwa maiti hizo zimehifadhiwa katika hospitali mbalimbali zikiwamo Muhimbili na Mwananyamala.

“Kwa mfano wa mkazi wa Vingunguti, Mabula Mosses amevunjika mguu baada ya kuangukiwa na ukuta wa kiwanda cha FIDA HUSSEIN kilichopakana na nyumba yake ,” alisema Kamishna Kova.

Kwa mujibu wa Kova, Katika Kata ya Jangwani, zipo nyumba zinazokadiriwa kufikia kati ya 90 na 100 zimefunikwa na maji hadi juu ya paa. Wakazi takribani 250-300 walihama mapema baada ya taarifa hiyo ya Serikali. Huku watu wanaokadiriwa kati ya 25-30 nao wamejihifadhi katika Shule ya Sekondari Mchikichini.

Kamishna Kova alitaja waliofariki dunia juzi ni Shaaban Idd (73), Masumbuko Deograss (50-55), Rashid Hassan (36), Groly Mrema ambaye alikuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu aliyefikwa na umauti na mwili wake kuonekana katika Mto Kizinga Manispaa ya Temeke.

TMA

Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania, TAM, imetoa taarifa kukanusha uwepo wa taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuwa kuna viashiria vya Tsunami.

Hata hivyo, TMA ilidokeza kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zitakoma ifikapo Mei 20, mwaka huu.

Chanzo:Mwananchi

NO COMMENTS