Nkurunziza atua Burundi, waasi watatu wakamatwa.

0
446

150513155644_rais_nkurunzinza_624x351_bbc_nocreditRais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amewasili jijini Bujumbura ikiwa ni siku mbili baada ya waasi kutangaza kumuondoa madarakani na tayari majenerali watatu waliotangaza mapinduzi wamekamatwa huku wanajeshi 12 wakiuawa.

Awali, kulikuwa na taarifa kuwa kiongozi wa uasi huo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alikuwa amekamatwa pamoja na wasaidizi wake, lakini baadaye mshauri wa habari wa rais, Willy Nyamwite alisema alipewa taarifa zisizo sahihi.

Lakini wakati kukiwa na habari kuwa Meja Jenerali Niyombire amekamatwa, waasi hao wamesema wataendeleza vita dhidi ya majeshi ya Serikali kwa ajili ya kumuondoa Rais huyo ambaye anapingwa kutokana na kutangaza kugombea urais kwa mara ya tatu kinyume na katiba.

“Amekamatwa, alikataa kujisalimisha,” Gervais Abayeho, msemaji wa Rais Nkuruzinza aliliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters.

Hata hivyo, mitaa mbalimbali ya jiji la Bujumbura ilikuwa imetulia na zaidi walikuwa wakionekana askari wanaomtii Rais Nkurunziza wakiwa katika vizuizi, ikiwemo Barabara Kuu ya Kusini mwa Bujumbura.

Msafara wa Rais Nkurunziza ulionyeshwa kwenye televisheni ukiwasili jijini Bujumbura, ingawa picha hizo hazikumuonyesha Rais huyo ambaye alipitia kijijini kwake Ngozi kabla ya kwenda jijini humo akitokea Tanzania.

Mnadhimu wa Jeshi, Jenerali Prime Niyongabo, akizungumza kwa mara ya kwanza tangu majeshi yanayomtii Nkurunziza yadhibiti redio na televisheni ya serikali, alisema wanajeshi 12 wa upinzani waliuawa wakati wa mapambano ya kuwania kituo hicho juzi.

Alisema wanajeshi wengine 35 wa uasi walijeruhiwa na 40 wamejisalimisha.

Alisema wanajeshi wanne wa Nkurunziza walijeruhiwa.

Hali ya jijini Bujumbura ilikuwa shwari jana baada ya mapambano kutawala siku nzima ya juzi wakati majeshi yanayomtii Nkurunziza yalipokuwa yakipambana kukomboa sehemu muhimu.

“Tunatoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Bujumbura kufungua tena biashara zao. Hali sasa imesharejea kuwa ya kawaida baada ya kushindwa kwa waasi,” Meya wa Bujumbura, Saidi Juma aliliambia shirika la habari la China, Xinhua.

Baada ya kuwasili, Rais Nkurunziza alipewa taarifa fupi ya mapinduzi na hata jinsi jeshi lilivyofanikiwa kuzima uasi na kutwaa tena miji ya Bujumbura.

“Rais Pierre Nkurunziza sasa yuko Burundi,” Msemaji wa Serikali, Willy Nyamitwe alisema.Kusoma zaidi bofya
“Hicho ndicho tunachoweza kusema kwa sasa.”

Jenerali Cyrille Ndayirukiye, msaidizi wa kiongozi wa mapinduzi hayo, alikiri kuwa jitihada za kuuangusha utawala wa Nkurunziza zimeshindikana.

“Binafsi, nakiri kusema, mipango yetu imekwama,” alisema Jenerali Ndayirukiye.

“Tulipambana tukijua kuwa tutaungwa mkono na jeshi.”

Wakati mapinduzi hayo yakifanyika, Nkurunziza alikuwa Tanzania kwa ajili ya mkutano wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi ulioibuka baada ya kiongozi huyo kutangaza kuwa atagombea urais kwa kipindi kingine cha tatu, kitu ambacho wapinzani wake wanasema ni kinyume cha katiba.

Mkurugenzi wa kituo kimoja cha redio, Jerome Nzokirantevye alisema askari wanaomtii Nkurunziza wameshadhibiti sehemu zote muhimu za Bujumbura, ikiwa ni pamoja na kituo cha redio na televisheni ya Serikali na Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.

Tangu kuanza kwa machafuko hayo, zaidi ya Warundi 100,000 wamekimbilia Tanzania, Rwanda na Uganda.

‘Wanamapinduzi’ wakamatwa

Majenerali wa kijeshi walioendesha jaribio la mapinduzi, tayari wametiwa mbaroni ikiwa ni saa chache baada ya Rais Nkurunziza kurejea nyumbani akitumia njia ‘zisizofahamika’.

Hata hivyo, ripoti zilisema kuwa kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Godefroid Niyombare alitoroka muda mfupi baada ya kuzingirwa na vikosi vya askari wanaomtii Rais Nkurunziza.

Inasadikika kuwa jenerali huyo amejificha kusini mwa mji wa Bujumbura na kwamba wapiganaji wake wanaendelea kushikiliwa.

Maofisa wa jeshi walisema kuwa bado wanaendelea kumsaka jenerali huyo ambaye awali alikiri kuzidiwa nguvu kiasi cha kuonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa maisha yake.

Akizungumza na Shirika la Habari la Ufaransa, AFP mapema jana, Jenerali Niyombare alisema kuwa jaribio la kuiondoa serikali iliyoko madarakani limeshindwa na wapiganaji wake walianza kujisalimisha.’

Naye msemaji wa waendesha mapinduzi hayo, Venon Ndabaneze alikiria pia kushindwa kwa jaribio lao akisema kuwa baadhi ya wapiganaji wao walikamatwa na vikosi vya serikali. Miongoni mwa waasi wanaoshikiliwa ni pamoja na msaidizi wa kiongozi wa mapinduzi hayo, Cyrille Ndayirukiye.

Marekani yawaonya raia wake

Marekani imewaonya raia wake kwenda nchini Burundi na kuwataka wale walioko ndani kuondoka haraka iwezekanavyo. Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa Burundi inakabiliwa na hali mbaya ya usalama, hivyo ni muhimu kwa raia hao kuchukua tahadhari mapema.

Taarifa hiyo iliwataka raia wote wa Marekani kutotembea ovyo na hata wale wanaotaka kuondoka kuangalia maeneo ambayo ni salama,” inasema taarifa hiyo.
Hata hivyo, mitaa mbalimbali ya jiji la Bujumbura ilikuwa imetulia na zaidi walikuwa wakionekana askari wanaomtii Rais Nkurunziza wakiwa katika vizuizi, ikiwemo Barabara Kuu ya Kusini mwa Bujumbura.

Uchaguzi Mkuu palepale

Utawala wa Rais Nkurunziza umesisitiza kuendelea na shughuli za Uchaguzi Mkuu ukisema kuwa utafanyika kama ulivyopangwa
Chanzo:Mwananchi

NO COMMENTS