Nani kuwa waziri mkuu?

0
664

Waziri mkuu wa sasa Mizengo Pinda je atarudishwa?
Habari kutoka ndani ya serikali, kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi zinaeleza kuwa pia Rais Kikwete anaelezwa huenda akafanya mabadiliko makubwa katika baraza lake la mawaziri ikiwamo kuunda baraza dogo la mawaziri ili kupunguza matumizi ya serikali na kuelekeza fedha nyingi kwenye shughuli za maendeleo.

Rais Jakaya Kikwete yupo kwenye hatua za mwisho kuunda serikali yake, ambayo wachambuzi wa mambo wanaeleza kwamba huenda ikawa na mabadiliko makubwa kuondoka kasoro zilizojitokeza miaka mitano iliyopita.

Wanaotajwa kwamba huenda wakaukwaa uwaziri mkuu katika ngwe hii ya pili ya Rais Kikwete ni pamoja na Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Mizengo Pinda, Samwel Sitta na John Magufuli.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini wanasema kuwa Pinda anaweza kurejeshwa katika kiti hicho kutokana na rekodi yake ya uadilifu, kutokuwa katika makundi na kutohusika katika kashfa ya aina yoyote na pia kutokuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, ikiwamo hatua yake ya kuzuia semina na safari za mara kwa mara za viongozi wa serikali nje ya nchi.

Na Mh. Sitta ametajwa kuwa anaweza kuupata uwaziri mkuu ikiwa ni njia ya Rais Kikwete kumfariji baada ya Kamati kuu ya CCM kumwengua kuwania uspika lakini pia inaelezwa kuwa ni njia mojawapo ya kuupoza umma ambao umeonyesha kusikitika kwa kunyimwa nafasi ya Bunge, ili kurejeshea serikali yake imani kwa wananchi.

Sitta anakumbukwa kwa kuliendesha Bunge kwa kiwango cha hali ya juu na kuruhusu mijadala wazi na kuchangia kuibuka kwa kashfa ya Richmond ambayo ilitikisa serikali baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu kwa kuwajibika na pamoja na mawaziri wawili walioiongoza Wizara ya Madini na Nishari kwa nyakati tofauti wakati wa mchakato kwa kuipitisha zabuni iliyoipa ushindi tata kampuni ya Richmond.

Mijadala mingine ambayo ilitiyotikisa nchi iliyojadiliwa bungeni ni wizi wa fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje katika Benki Kuu (EPA) na mikataba mibaya katika sekta ya madini.

Aliyekuwa Waziri wa Mifungo na Uvuvi, Dk John Magufuli anatajwa kuwa anaweza kupata nafasi hiyo nyeti kutokana na utendaji wake makini wa kazi kwani ana rekodi nzuri ya kufanya vizuri katika wizara zote alizopangiwa na hana kashfa wala makundi ndani ya CCM.

Saa chache zijazo tutamjua nani waziri mkuu wa serikali ya awamu ya nne na huko Dodoma inaripotiwa kuwa gumzo kubwa hivi sasa ni nani atateuliwa kuwa waziri mkuu.

Mh. Samwel Sitta ametajwa huenda akachukua nafasi hiyo.

NO COMMENTS