Mwanzo mzuri kwa jaji Kaganda

0
451

Jaji mstaafu Salome Kaganda(kulia) akiapishwa na rais Jakaya Kikwete. Ikulu mjini Daressalaam.
Kitendo cha hivi karibuni cha kamishna mpya wa maadili ya viongozi wa umma jaji mstaafu Salome Kaganda kutangaza kuwa atapambana na viongozi wasiotaja mali zao ni cha kizalendo, kilichojaa ushupavu na kuonyesha moyo wa uchapa kazi wa kweli.

Jaji huyu alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi amesema kuwa ” kuna viongozi waliotumia mwanya wa baadhi ya mapungufu katika usimamizi wa sekretarieti hiyo miaka iliyopita, sasa wajue watakumbana na msumeno wa sheria.” Aliongeza kuwa “inawezekana kulikuwepo na mapungufu (kwenye uongozi wa sekretarieti) miaka iliyopita, lakini mimi nitajitahidi nisiingie kwenye mapungufu hayo”.

Hii inaonyesha wazi kwamba kweli mapungufu yalikuwapo kwani kuna viongozi wangapi waliojitokeza hadharani kutaja mali zao tangu Rais Ben Mkapa alipofanya wakati wa utawala wake? viongozi wengi hawajataja mali zao na wachambuzi wameeleza wazi kuwa kumekuwa na udhaifu katika sekretariat iliyopita.

Hivyo basi jaji Kaganda ameweka wazi kwamba yeye hatakubali kuona mapungufu na kutangaza atahakikisha sheria hiyo inafuatwa kwani iko wazi, kwamba viongozi wote wa umma wanatakiwa kutaja mali zao na inaenda kwa kiapo.

Kumekuwa na shutuma nyingi kwa viongozi wa umma kujilimbikizia mali zinazopatikana kinyume cha sheria na ndio maana inakuwa ni mtihani mkubwa kuingia hadharani na kuzitaja mali hizo lakini kama zimepatikana kihalali wasiwasi wa nini? kazi kwako Jaji Kaganda yetu sisi ni macho kuona utekelezaji wa sheria hiyo wa dhati na si kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Mpaka sasa Jaji Kaganda ameonyesha kuwa kweli amedhamiria kutelezwa kwa sheria hiyo kazi kwenu viongozi wa Tanzania huru.

NO COMMENTS