Meneja wa zamani wa Uganda Cranes ahukumiwa miaka 10 jela.

0
753

Mahakama nchini Uganda imemhukumu aliyekuwa meneja wa timu ya taifa ya kandanda Chris Mubiru, miaka 10 gerezani kwa makosa ya kufanya ngono na wanaume.

Jaji wa mahakama ya Buganda Road Flavia Nabakooza pia amemwamuru Mubiru kuwalipa waathirika fidia ya shilingi milioni 50 kila mmoja, na kueleza kwamba ushahidi uliotolewa mahakamani unatosha na kuiridhisha mahakama kumhukumu Mubiru.

Katika uamuzi wake, mbele ya mahakama iliyofurika, jaji Flavia Nabakooza ameeleza kwamba ushahidi uliotolewa mahakamani unatosha kuamini kwamba Chris Mubiru alikuwa na mazoea ya kufanya tendo la ngono na wanaume bila ya idhini yao, akiwemo mwathiriwa kwa jina Emmanuel Nyanzi.
Jaji Nabakooza pia ameeleza mahakama kwamba vipimo vilivyofanywa katika maabara ya serikali vimethibitisha kwamba vitu vilivyopatikana nyumbani kwake Mubiru yakiwemo mafuta na dawa za kutuliza maumivu, vinatumiwa na mashoga.

Mawakili wake Chris Mubiru wakiongozwa na Isaac Semakadde, wamesema watakata rufaa.

“mteja wetu Chris Mubiru hajaridhia uamuzi wa mahakama na ametuomba tukate rufaa katika mahakama kuu ya Uganda” amesema Isaac Semakadde.
Jaji Nabakooza, ametumia ibara ya 145 sehemu ya (a) ya sheria za Uganda, yaani Penal code, kumhukumu Mubiru kwa makosa ya Ushoga, lakini wakili wake Mubiru wanasema mahakama imekosea.

“tumeona mahakama imekosea kabisa lakini leo siwezi kuzungumzia sana” aliongezea kusema Isaac Semakadde.Kusoma zaidi bofya

Mwenyekiti wa muungano wa wanaopinga ushoga nchini Uganda Muhubiri Solomon Male, ameelezea furaha yake baada ya hukumu hiyo.
“ nina furaha sana hii leo kwamba huyu jamaa ambaye ni shoga, Chris Mubiru, ambaye amekuwa akiwalenga wavulana wenye umri mdogo, wachezaji soka, vipaji vinavyochipuka, amehukumiwa miaka 10 gerezani na kuamrishwa kuwalipa waathiriwa fidia ya shilingi milioni 50. Ni kesi ya kihistoria, hasa katika nchi ambayo wabunge wamekuwa wakiwadanganya raia kwamba hakuna sheria kuwahukumu mashoga” amesema mhubiri Solomon Male.

Lakini baadhi ya raia wanahisi kwamba hukumu ya miaka 10 gerezani aliyopewa Mubiru haitoshi.

“nadhani wangeongeza iwe kama miaka ishirini hivi. Ni vizuri sasa watu wajue kwamba hapa Uganda kuna sheria za kuwahukumu mashoga na hakuna haja ya kutunga sheria zingine” .

Chris Mubiru alikamatwa tarehe 15 mwezi Desemba mwaka 2009. Kesi hiyo imechukua muda mrefu kuamuliwa baada ya kutokea mjadala kote duniani kuhusu haki za mashoga.

Nchini Uganda, kosa la Ushoga lina hukumu ya maisha gerezani.

NO COMMENTS