Lowassa, Sitta waanza kwa mbwembwe.

0
509

lowasa+pichaMakada wanaoomba kupitishwa na CCM kuwania urais jana walianza kusaka wadhamini kwa staili ya aina yake baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kuibuka na basi la kifahari atakalotumia kuzunguka mikoani, huku Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akitua Mwanza kwa ndege.

Sitta, ambaye alitangaza nia yake ya kuwania urais juzi, jana alikuwa miongoni mwa makada watatu waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo kwenye ofisi za makao makuu ya CCM mjini Dodoma kabla ya kuanza kusaka wadhamini.

Wengine waliochukua fomu ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Titus Kamani na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Wanaochukua fomu hizo za CCM wanatakiwa kutafuta wanachama kwenye mikoa 15, huku 10 ikiwa ya Tanzania Bara na mitano ya Zanzibar na wanatakiwa wapate wadhamini 450 kwa mikoa hiyo na mwisho wa kurudisha fomu ni Julai 2 wakati vikao vya mwisho kuteua mgombea vitafanyika Julai 12.

Sitta, ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alianza kutafuta wadhamini mjini Dodoma na alitarajiwa kuendelea na kazi hiyo kwenye mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe na Mbeya, lakini kilichovutia zaidi ni basi alilosema amekodi aina ya Yutong ambalo lina sehemu ya kukaa kama sebule.

Sitta na basi lake

Sitta alifika katika jengo la ofisi hizo za CCM akiwa ndani ya basi hilo aina ya Yutong, ambalo alisema sehemu yake ya ndani ilibuniwa na mwanaye.

Ndani ya basi hilo kuna kochi moja kubwa ambalo linaweza kutumika kama kitanda, kiti cha ofisini na meza ndogo iliyopambwa na picha yake na maneno “viwango mwaka 2015-2020”.

“Hivi vyote ni vitu vya nyumbani kwangu, kijana wangu anaitwa Ben alibuni namna (ya kuviweka kwenye basi). Sikutumia gharama yoyote zaidi ya kukodisha basi,” alisema Sitta akiwa ndani ya basi hiyo na mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage.Kusoma zaidi bofya

Alisema aliamua kutumia basi hilo la abiria ili apunguze gharama za utafutaji wa wadhamini katika mikoa 18 anayotaka kwenda kuwatafuta.Kusoma zaidi bofya

“Unajua nina marafiki zangu kama 11 nataka niwe nao sasa kutumia usafiri wa magari ni gharama ndio maana tukaamua kufanya hivi,” alisema Sitta na kuongeza kuwa katika safari zake hizo atakuwa akisafiri usiku.

Vipaumbele vya Sitta

Sitta aliianza ziara hiyo ya kutafuta wadhamini katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa huku leo akiwa katika mikoa ya Njombe na Mbeya.

Mjini Dodoma, akizungumza baada ya kuchukua fomu, Sitta alirejea tena vipaumbele vyake vitano vinavyomfanya kuwania nafasi hiyo ya juu.

Sitta, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema sababu ya pili ni changamoto katika Katiba Inayopendekezwa.

Alisema Katiba hiyo bado ina changamoto lakini yeye anaamini ndio msingi wa kulivusha Taifa kwenda mbele.

“Bado kuna wazalendo wa pande zote mbili wanaoweza kukaa pamoja na kuhakikisha kuwa mchakato wa Katiba unaisha vizuri na inapigiwa kura bila tatizo lolote,”alisema.

Alisema anajihisi kuwa anajukumu kama Mtanzania anayefahamu Katiba Inayopendekezwa.

Kipaumbele kingine ni kupambana na rushwa kwa kuhakikisha kutenganisha biashara na uongozi.

Alisema endapo atafanikiwa kuipata nafasi hiyo, itaandaliwa sheria maalumu ambayo itawalazimisha watu kuchagua kati ya biashara na uongozi.

“Endapo atakuwa na biashara basi akubali kuikabidhi kwa utaratibu wa kisheria kwa mtu atakayeiendesha na atakaporudi aweze kuiendesha tena,”alisema Sitta.

Alisema na ndio maana katika kipindi hiki kumezuka watu waliokuwa wa kawaida lakini sasa ni mabilionea kwasababu ya kuchanganya biashara na uongozi.

Sitta alisema katika mapambano hayo, Tume ya Maadili itapewa nguvu ambazo hazitahojiwa mahali popote pale na kuendesha mambo yake kwa uwazi.

“Na mali yoyote isiyoelezeka lazima itaifishwe, rushwa huwezi kuichezea chezea hivi kwasababu rushwa inadhoofisha maendeleo,”alisema.

Alitaja kipaumbele chake kingine kuwa ni kuleta uhusiano mzuri na motisha baina ya wazalisha mali, wakulima na serikali yao.

Alisema hakuna uhusiano mzuri kati ya serikali na wazalishaji mali na kwamba uchumi hauwezi kukua bila kuwa na uhusiano huo.

“Jambo la mwisho ni kuimarisha chama, huwezi kuwa na watumishi hawaridhiki, mishahara yao inalipwa kwa tabu, malipo shida na chama tawala kinapochukua sura hiyo inakuwa vigumu kusimamia watendaji…Hii ni kichwa chini miguu juu,” alisema Sitta.

Alisema hali hiyo imewaharibia katika chama kwa kuwa na baadhi ya wafanyabiashara kudhani wao ndio chama baada ya kukisaidia.

Alisema kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano, ataimarisha chama kiuchumi.

Lowassa atua Mwanza

Mjini Mwanza jana, Lowassa alianza hatua hiyo ya mwisho ndani ya CCM kuelekea kugombea urais kwa kupata mapokezi makubwa yaliyomshawishi kusema “kama ni mpira, tayari nimeshinda kwani sijawahi kupata mapokezi makubwa kama haya Mwanza”.

Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Elias Mpande alimkabidhi Lowassa fomu iliyokuwa na wadhamini 1,671.

Hata hivyo, mgombea anatakiwa apate wadhamini 30 kila mkoa na kupata idadi ya jumla ya wadhamini 450 kwa mikoa 15, kwa mujibu wa kanuni za CCM.

“Nina sababu kuu mbili za kusema kwamba nadeka na kama ni mpira nimeshinda. Mapokezi niliyoyapata hapa Mwanza hayajawahi kutokea, lakini hii ni faraja kubwa ya pekee kwangu,” alisema Lowassa baada ya kukabidhiwa fomu hiyo.

“Leo sitasema sana, lakini nawaomba wana-CCM tujenge mshikamano wa pamoja kukabilina na vita ya watu watakaokomba rasilimali za Taifa.”

Pia, alisema Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakuwa mgumu tofauti na uliopita na kwamba, ni mtihani kwa CCM kuteua mtu makini atakayaweza kulinda rasilimali za nchi.

Lowassa alisema huu ni wakati wa CCM kujenga mshikamano wa pamoja na kukabiliana na watu ambao wanaweza kukomba rasilimali za nchi.

Mapokezi, ulinzi

Lowassa, ambaye aliwasili Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 6:00 mchana na kupokelewa na wafuasi wa chama hicho huku kukiwa na ulinzi mkali, baadaye alielekea Ofisi ya CCM kusaini kitabu cha wageni.

Umati wa watu ulifurika kwenye ukumbi huo wakiwamo viongozi mbalimbali wakiongozwa na maandamano ya waendesha pikipiki, wanaojulikana kama bodaboda.

Baada ya kutoka ofisi hizo, Lowassa, akilindwa na mabaunsa waliovalia suti nyeusi, alitembea umbali wa mita 150 hadi ukumbini, huku akishuhudiwa na watu wengi waliokuwa pembeni mwa barabara wakishangaa msafara wa mbunge huyo wa Monduli ukiongozwa na gari lenye rangi nyeusi.

Polisi wa Kikosi cha Usalama barabarani walikuwa wakihahaha kuongoza magari na kupunguza foleni kutoka Barabara ya Uwanja wa Ndege kuingia katikati ya mji, huku ving’ora vikitawala.

Kuhusu gesi

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, Lowassa alisema nchi imebarikiwa kupata gesi ambayo ni mtaji mkubwa kwa Taifa, lakini watakuja watu kutoka mataifa ya nje na kuisomba hivyo anahitajika mtu makini wa kuweza kuhimili hali hiyo.

Bila ya kuwataja majina, Lowassa alisema wapo wakubwa wengi ambao watataka wamshike pua kiongozi atakayekuwa madarakani, ili kumnyamazisha na kupata fursa ya kuchukua rasilimali hiyo muhimu.

“Hii gesi tunaweza kusema tumepata, tukafurahia kumbe ni laana tusipokuwa makini. Kuna watu wanataka kuja kusomba utajiri wetu, inaleta ushindani mkubwa wapo wakubwa watataka wamshike pua kiongozi na kumpeleka mbele wanapotaka wao,” alisema Lowassa.

Alisema iwapo CCM ikimpitisha mtu makini, watu hao hawataweza kupokonya rasilimali hiyo kwani wameshindwa kwa awamu nne zilizotangulia kutokana na viongozi hao kuwa makini na rasilimali za Taifa.

Daftari la wapiga kura

Lowassa alisema siri ya kumpeleka mtu Ikulu ni kura, hivyo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi hao kujitokeza kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Wapigakura.

“Tofauti na hapo hata mapokezi haya makubwa na yenye furaha mlionionyesha yatakuwa ni bure, kwani hatutaweza kushinda uchaguzi huo maana utakuwa na ushindani mkubwa,” alisema.

Muda wote wakati akizungumza wananchi walikuwa wakimshangilia ndani na nje ya ukumbi, kutokana na ukumbi huo kuwa mdogo baada ya kufurika walilazimika kuchungulia kupitia madirishani.

Kabla ya kuanza kushukuru, Lowassa aliamka kwenye kiti na kuanza kucheza muziki wenye kibwagizo cha “sasa kumekucha jogoo kishawika Dodoma” ulioimbwa na marehemu Kapteni John Komba huku ukumbi mzima ukicheza.

Viongozi wampamba

Lowassa aliambatana na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk Raphael Chegeni, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka mikoa mbalimbali.

Masha atoa neno

Awali, akizungumza kabla ya kukabidhiwa majina ya wadhamini kwa Lowassa, Masha aliwaomba wakazi wa Mwanza wasimwangushe na kwamba, wamuunge mkono Lowassa kwani nchi inamhitaji.

“Sisi kama Wanamwanza tuna imani kubwa na Lowassa, ni vyema tukamuunga mkono kwa pamoja, kwani nchi inamhitaji. Tumefarijika Mwanza kuwa ya kwanza kwa Lowassa kuja kutafuta wadhamini hii ndiyo ngome yake,” alisema Masha.

DC Nyamagana

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga alisema hajatumwa na mtu kwenda kushuhudia tukio hilo, bali sherehe hizo zimefanyika ofisini kwake hivyo amelazimika kuwapo.

Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani alitangazia nia yake ukumbini hapo lakini Konisaga hakujitokeza.

“Mheshimiwa Lowassa mimi hapa nimekuja kikazi, naomba ifahamike sijatumwa na mtu hili ni eneo langu la kazi, hivyo imenibidi niwepo hapa kuimarisha ulinzi,” alisema Konisaga.

Wassira aanzia Dodoma

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ameanza kutafuta wadhamini katika mbio za kuelekea Ikulu katika mkoa wa Dodoma.

Akizungumza jana, Wasira alisema kuwa baada ya kuchukua fomu, ameanza kibarua hicho Dodoma mjini na baadaye kuendelea mikoa mingine.

“Nimeanzia Dodoma na baadaye nitakwenda mikoa ya Arusha, Singida, Tanga, Manyara na Kilimanjaro kwa ajili ya kupata watu wa kunilinda katika safari yangu,” alisema Wasira aliyesema akiingia madarakani kati ya mambo anayoyaamini ni uadilifu.

Akizungumza na Mwananchi Wasira alisema kuwa tayari ameshapata wadhamini katika mikoa hiyo huku safari yake ikiendelea na ikitimia kwa mafanikio makubwa.

Siyantemi naye Dodoma

Kwa upande wa Amos Siyantemi amesema ameshatafuta wadhamini katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.

Alisema anaendelea kutafuta wadhamini katika mikoa hiyo na amekamilisha na leo atakuwa Shinyanga, Mwanza na Mara na akimaliza mikoa ya Kanda ya Ziwa ataendelea katika mikoa mingine.

Dk Kamani

Baadaye Dk Kamani alichukua fomu na kusema katika kukabiliana na changamoto za afya, ajira, uchumi yanahitajika mawazo mengine na kwamba yeye kwa kushirikiana na viongozi wenzake ndani ya CCM na serikali watakayoiunda wataongeza kasi katika kupambana na changamoto hizo.

Dk Kamani alisema akifanikiwa kuipata nafasi hiyo ataangalia tatizo la ajira, makundi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na wazee wastaafu.

“Makundi makubwa ya wafanyakazi ambayo bado hali zao zinatakiwa kuangaliwa, yataangaliwa,” alisema.

Alisema pia ataongeza fursa ya kuondoa umasikini hasa kwa kuzingatia kuwa asilimia 80 Watanzania wanaishi vijijini.

Alisema ili kuuondoa umasikini, atahakikisha wakulima wanafanya kilimo cha kisasa kwa kuwezesha kupata pembejeo.

“Ni lazima kuongeza usindikaji kwa kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo na hii itasaidia katika kupunguza tatizo la ajira nchini pia,”alisema Dk Kamani.

Alisema kwa kuongeza thamani ya mazao, kutaongeza bei na hivyo kuongeza mapato.

Alisema ili kuongeza mapato ya nchi yeye na wenzake wataimarisha sekta nyingine kama madini, kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na mali kale. Pia alisema atajitahidi kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi jirani na nchi nyingine duniani.

“Mahusiano itakuwa ni msingi wa kujenga uchumi wetu. Balozi zetu tutaimarisha ili ziweze kuwa wawakilishi wazuri wa kutafuta maarifa, teknolojia na masoko ya bidhaa zetu,”alisema.

Alisema anajua kuwa mambo yote yanahitaji fedha, hivyo mikakati yake ni kuimarisha viwanda, sekta ya uchukuzi ambazo zitasaidia kuingiza fedha nyingi ndani ya nchi. Alisema pia wataimarisha wafanyabiashara ndogo ndogo ili waweze kulipa kodi.

Pia alisema akipata nafasi hiyo atapambana na rushwa ambayo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo na kwamba katika awamu yake ya uongozi mchwa wanaotafuna fedha hawatakuwa na nafasi.

Muhongo

Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo ambaye alikuwa wa kwanza kuchukua fomu jana, alisindikizwa na gari moja aina ya Toyota Hiace ambalo lilibeba wapambe waliovalia mavazi ya kawaida na hakutaka kuongea na waandishi wa habari kama ilivyo kuwa juzi kwa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Hata hivyo, alipoulizwa ana imani vipi na mchakato wenyewe, Profesa Muhongo alisema Wana-CCM wanafahamu kuwa chama hicho kina demokrasia kubwa na ndio maana wanachukua fomu na kuzunguka nchini nzima kudhaminiwa ili kuonyesha imani ya awali.

“Nafasi yangu ni muhimu kwa sababu Watanzania wamechoshwa na umasikini, wamechoka kazi kufanywa kwa mazoea. Wanataka mawazo mapya, wanataka watu wapya, wanataka ubunifu mpya, wanataka watu wenye uzoefu kimataifa na kimataifa,”alisema.

Alipoulizwa ni mgombea gani ambaye anahofu naye zaidi kati ya wale walijitokeza kuwania nafasi hiyo, Profesa Muhongo alisema yeye hahofii yeyote na kwamba Watanzania wenyewe ndio watajua nani ana hofu na nani anawafaa zaidi.

“Si vizuri kuongelea watu, mimi sipendi kuongelea watu,”alisema Profesa Muhongo na kuondoka katika eneo la jengo hilo.

Chanzo:Mwananchi

NO COMMENTS

  1. Wamekuwa wakisema mengi sana sasa kukosoa serikali yao. Hivi hao walikuwa wapi wakati serikali inafanya utumbo huo wote. Aaa hakuna hata mmoja aliye msafi hapo.