Kingunge anusa mchezo mchafu urais ndani ya CCM.

0
720

pic+kingungeMwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru amesema anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza kuwa ni ishara mbaya.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais wa awamu zote nne, pia, bila kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kujibu kauli ya makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliyekaririwa akisema kuwa mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.

Kingunge, ambaye amejitokeza hadharani kumpigia debe Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka wadhamini mkoani Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani Kinondoni.

Hadi sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM ni 41 baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana akisema atamudu kupata wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano zilizosalia. Akizungumza katika mkutano wa kusaka wadhamini ulioandaliwa kwa ajili ya Lowassa wilayani Kinondoni jana, Kingunge alipingana na kauli ya Mangula kuwa mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi mwenyewe akisema chama hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na nje.

Siku tatu zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa anatakiwa kunadiwa na chama.

Lakini Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema chama hicho kimeweka utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza kuwahukumu wagombea kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi kuwahukumu wagombea kabla katika chaguzi zilizopita.

“Mchakato ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema Kingunge ambaye aliibuka Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli zake jijini Dar es Salaam.

“Nimemsikia kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi hapa, nikamuona kwenye televisheni anasema mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi, ananadiwa na chama.

“Nikasema eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze yeye na wenye fikra kama hizo kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu wetu; kwanza, mwanachama anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima ajinadi ndani ya chama, ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa katiba na taratibu zetu. Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”

Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.

“Si vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama wakaanza ama wakaendelea kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi. Kama wana mashaka tupo tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku akishangiliwa na mamia ya watu.

Kingunge alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa Dodoma alisema chama kinatafuta mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho ili kuweza kushindana na vyama vingine.Kusoma zaidi bofya

“CCM inamtafuta mtu ambaye anakubalika ndani na nje ya chama. Wale wanaofanya jitihada za kuunda mazingira ya kukitafutia chama kushindwa, wanataka historia iliyotukuka ya CCM iishe katika awamu ya nne,” alisema.

”Tunapozungumzia suala la urais kwa sababu linahusu watu, tusianze kukaa kwenye mizengwe. Kwanza tuwaulize watu wanamtaka nani atayeweza kuwatatulia matatizo yao.”

Kingunge alisema idadi ya wagombea nafasi ya urais waliojitokeza kwa tiketi ya CCM ni wengi na kwamba idadi hiyo ambayo alisema haijapata kutokea katika historia ya chama, inaashiria kuwa kuna jambo linataka kufanyika.

“Nasema hao wagombea wapo wengi, sasa wenye macho wanaona watu wanasema nini. Matumaini yangu ni kwamba watu watatuliza vichwa kukubali ukweli na kuachia utaratibu wetu uendelee unavyotakiwa,” alisema.

Aliwataka viongozi ndani ya CCM kutokiuka taratibu za chama hicho za kumteua mgombea, kuwataka kutumia utaratibu uliozoeleka na ambao ulitumiwa katika chaguzi zilizopita.

Alisema Watanzania wana changamoto nyingi na kwamba tangu mwanzo chama hicho kimekuwa kikilia na umasikini unaolikabili taifa, huku akisisitiza kuwa mwarobaini wa kuondoa hali hiyo ni Lowassa.

Kingunge alisema licha ya marais wa awamu zote kufanya mambo mengi, nchi kwa sasa inahitaji kiongozi atakaye ondoa umaskini.

“Na linawezekana hilo, nasema tunapozungumzia suala zima la urais tunazungumzia hatma ya Watanzania. Tusifanye mchezo nalo, hatuwezi kukaa tukasema yeyote tu anaweza. Hiyo sio lugha ya watu makini. Kauli hiyo itasemwa na walionacho, lakini wasionacho hawawezi kusema hivyo,” alisema Kingunge.

Kauli ya Lowassa

Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa wilayani Ilala, Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam, Lowassa alirejea kauli iliyotolewa na Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1995, kwamba watu wanataka mabadiliko na wakiyakosa ndani ya CCM, watayatafuta nje ya chama hicho.

“Mimi nitayaleta haya mabadiliko nikiwa ndani ya CCM. Nagombea urais kwa sababu nauchukia umasikini na nitaunda serikali ya kusaidia wanyonge, kuwafukuza machinga, mamantilie na waendesha bodaboda ni upuuzi. Watu wanatafuta riziki tunawafukuza inatakiwa tuwawekee mazingira mazuri,” alisema na kushangiliwa kwa nguvu.

Alisema anauchukia msongamano wa magari jijini Dar es Salaam na iwapo atakuwa Rais atalimaliza tatizo la foleni katika jijini Dar es Salaam kwa miezi sita.

“Kutakuwa na waziri anayeshughulika na jiji la Dar es Salaam tu kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya. Yeye akiamka tu akili yake yote ni kushughulikia changamoto za jiji hili,” alisema Lowassa ambaye mara kwa mara alikuwa akiwaimbisha wananchi wimbo wa ‘mchakamchaka’, huku akisisitiza kuwa ataiongoza serikali yake kwa mtindo wa mchakamchaka akisema ambaye hataweza atakaa pembeni.

Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura ili wapate fursa ya kumchagua iwapo atapitishwa na chama hicho kugombea urais, huku akiwataka wamuombee kwa maelezo kuwa Mungu ndiye anayepanga kila kitu.

“Mrema (Augustine) alikuwa maarufu sana mwaka 1995 mpaka gari lake likawa linasukumwa na wananchi, lakini katika kura za urais hakushinda. Jiandikisheni ili tufanikishe safari ya matumaini,” alisema.

Lowassa alisema kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaomuunga mkono anaona kama tayari ameshashinda huku akisisitiza kuwa ameshawafunga goli wagombea wenzake kama anavyofanya mchezaji wa timu ya soka ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

“Kati ya wagombea wote hakuna mwenye uzoefu ndani ya CCM kama mimi. Kumbukeni rais ndiye mwenyekiti wa CCM,” alisema.

Aiteka Dar

Lowassa aliwasili katika uwanja wa ndege wa zamani (Terminal 1), saa 2:00 asubuhi akitokea mkoani Arusha.

Mwenyekiti wa CCM wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida alisema wanachama wa mkoa huo waliojitokeza kumdhamini ni 212,150, kati yao kutoka Kinondoni ni 95,251, Temeke (72,100) na Ilala (44,799).

Afananishwa na mtume, Yesu

Akimkaribisha Lowassa Dar es Salaam, Madabida alimfananisha waziri mkuu huyo wa zamani na Mtume Muhammad ambaye alikuwa akitangaza dini lakini alikuwa akipingwa na watu wake wa karibu na kufafanua kuwa kutokana na hali hiyo Mungu alimueleza kuwa hatamuacha na atakuwa pamoja naye.
Chanzo:Mwananchi

NO COMMENTS