Kesi ya Ghailani yaleta utata mkubwa Marekani

0
440

Mtuhumiwa wa mabomu ya Daressalaam na Nairobi Ahmed Ghailani
Tangu mwanzo, kesi ya serikali ya marekani dhidi ya Ahmed Ghailani, raia wa Tanzania, ilichukuliwa kuwa ni mtihani kwa mfumo wa mahakama ya kiraia ya Marekani ikiwa utaweza kuwahukumu wageni wanaoshukiwa kuwa ni magaidi. Na hivi sasa hukumu imeshatolewa, na kila mtu anachukulia jinsi alivyo ridhika na kesi hiyo.

Miongoni mwa mashtaka 285 alioshtakiwa kuhusiana na mashambulio ya 1998, baraza la mahakama lilimpata Ghailani kuwa na hatia na shitaka moja tu, nalo ni njama ya kuharibu mali ya Marekani.

Wakili wake Peter Quijano alikua na furaha na kumshukuru hakimu na baraza la mahakimu kwa kesi anayosema ilikuwa ya haki.

Anasema, “hata kabla ya uamuzi kutolewa alikuwa na imani na mfumo wa sheria na alikua na imani na kesi zinazosimamiwa na baraza la mahakimu”.

Watu ambao hawakuridhika sana ni wabunge wa Marekani ambao kwa muda mrefu wamepinga nia ya utawala wa Obama kuwafungulia mashtaka watuhumiwa wa ugaidi wanaoshikiliwa katika jela ya Guantanamo Bay, Cuba katika mahakama ya kiraia badala ya koti za kijeshi.

Seneta Joe Liberman, mwenyekiti wa kamati ya usalama wa ndani katika baraza la Senet anasema, “ninadhani hukumu ya Ghailani haitoshitisha kabisa kesi za kiraia kwa wafungwa, bali ina sababisha kuwepo na uwezekano wa kutofanyika nyingi. Kwake yeye anasema wako vitani na watu wanaokamatwa katika vita ni lazima washikiliwe katia mazingira ya kijeshi.

Liberman ameiambia Sauti ya Amerika (VOA) kwamba, hukumu ya Ghailani haitatanishi tu kesi za siku zijazo bali pia inasababisha lengo la Rais Obama, la kufunga Guantanamo kuWa gumu kabisa kulifikia.

Kwa upande wake mbunge atakae kuWa Spika mpya wa Baraza la Wawakilishi kuanzia mwakani, mrepublican John Boehner hakuficha upinzani wake. Katika taarifa, Boehner amesema, hukumu ya Ghailani ni ushahidi zaidi kwamba, mpango wa kusikiliza kesi za watuhumiwa wa ugaidi katika mahakama ya kiraia ilikuwa ni kosa tangu siku ya kwanza. Alitoa wito kwa utawala wa Obama kubadili mkondo na kutowaleta wafungwa wa Guantanamo Bay kwenye ardhi ya Marekani na kuwafungulia mashtaka katika korti za kijeshi.

Makundi ya kutetea haki za binaadam na haki za kiraia yanachukua msimamo tofauti. Mkurugenzi wa Human Rights Watch mjini Washington, Tom Malinowski, anasema uwamuzi katika kesi ya ghailani unaonesha kwamba mahakimu wa kiraia na baraza la mahakimu wana uwezo kamili wa kuhukumu kwa haki hata ikiwa uamuzi haujaridhisha kila mtu.

Malinowiski anasema korti ya kijeshi huenda ingelitoa uwamuzi kama huo uliotolewa katika kesi ya Ghailani katika mahakama ya kiraia.

Akizungumza na waandishi habari msemaji wa White House Robert Gibbs alidokeza kwamba hukumu ya Ghailani ina adhabu kali ya kifungo cha miaka 20 jela bila ya msamaha na kwamba Ghailani hatokua kitisho tena kwa wa Marekani kutokana na hukumu hiyo. Amesema Rais Obama yungali na nia ya kuifunga Guantanamo, hata ikiwa mpango wake wa awali wa kuifunga jela katika kipindi cha mwaka moja tangu kuchukua madaraka umepitwa na wakati.-Chanzo cha habari www.voaswahili.com

NO COMMENTS