Je Tea Party wataweza kumwangusha Obama?

0
377
Rais wa Marekani Barack Obama
Barack Obama

Suala la vugu vugu la Tea Party limeleta sura mpya kwenye siasa za Marekani ambapo katika siku za karibuni vugu vugu  hilo limechukua nafasi ya pekee katika siasa za Marekani na hasa kumpinga Rais Barack Obama na sera zake kuanzia mabadiliko ya afya mpaka ya mfumo wa fedha na shutuma mbali mbali ikiwa ni pamoja na kumwita mjamaa na asiye raia wa Marekani. Si hivyo tu walikampeni dhidi ya Obama na wagombea wake katika nafasi mbali mbali kiasi cha kwamba Chama cha Democrat kilipoteza jimbo muhimu lililobadili msimamo kwenye uchaguzi wa mwaka 2008 la Virginia  kutoka Republikan na kumchagua Obama Mdemocrat ambapo Gavana wa jimbo hilo alirudi kuchaguliwa Mrepublikan na si hivyo tu hayo  hayakuishia hapo  yalienda New Jersey ambapo lile ni jimbo la wademocrat lakini la hasha walijikuta wakilipoteza kwa warepublikan ambapo alichaguliwa  Gavana mrepublikan Chris Christie pamoja na kampeni kali za Obama.

Sasa kutokana na hayo  nimezungumza na mtafiti na mchambuzi  wa kisiasa na mfasiri wa kujitegemea Professa John Mtembezi na kumuuliza kama Je vugu vugu hili litaweza kumwangusha Rais Barack Obama kwenye uchaguzi wa mwaka 2012. Na Profesa anaeleza yafuatayo:

Profesa John Mtembezi
Profesa John Mtembezi

Kuhusu Tea Party na uwezo wake wa kumwangusha Obama 2012, mimi binafsi sidhani wao peke yao wataweza kufanya hivyo. Kwanza tukumbuke kuwa Tea Party ni mseto wa watu kadhaa wenye itikadi, siasa, na mtazamo wa dunia nzima vinavyolingana. Lakini Tea Party yenyewe si chama cha siasa. Wengi wao hujiita “Marepublican” isipokuwa mara nyingi watu hao hao ndio wanaopinga vikali baadhi ya sera za chama cha Republican pamoja na wanasiasa wa chama hicho. Hivyo, vuguvugu lao la kisiasa, kwa kiasi kikubwa, ni kama uasi ndani ya chama cha Republican. Hivyo, upo uwezekano harakati za vuguvugu hilo zitahatarisha wanasiasa wa chama hicho kuchaguliwa tena mwezi wa Novemba.
Vilevile kupinga sera fulani fulani ni kazi rahisi; lakini kupendekeza ya kufanya ili kurekebisha hali fulani na halafu kulitekeleza pendekezo hilo ni tofauti na ni kazi ngumu zaidi.
Tuangalie masuala makuu mawili yaliyo muhimu sana kwao. La kwanza ni lile la ndoa ya watu wa jinsia moja. Nakubali kwamba walio wengi nchini humu hawapendi kuona ndoa za namna hiyo zifanywe halali. Lakini tusisahau kwamba haizidi miaka 25 iliyopita watu wengi nchini huku hawakupeda pia kuona ndoa baina ya mweusi na Mzungu, wengine wao wakidai eti ndoa ya namna hiyo inakwenda kinyume na mila, desturi, na matakwa ya Mwenyezi Mungu!
Mstari wa kitako ni huu: watu wanaoitwa “gay” katika nchi hii … yaani wasenge na wasagaji … wamezaliwa hapa, wamekulia hapa, wengi ni walipaji kodi kama Wamarekani wengine, wengine ni wanasiasa, na wengine wamewahi kuwa hata wanajeshi nyakati za vita. Ikiwa ni hivyo, basi swali la kimsingi linalofuatia ni: “Je, wao ni wananchi halisi wa Marekani au la?” Kama jibu ni la, wao sio wananchi, basi nadhani wenye kujibu hivyo waona itakuwa sawa kuwanyima haki za kiraia na kuwabagua na kuwadhulumu. Lakini tukikubali ya kuwa hao ni raia halisi wa nchi hii, basi wao hawana budi kupatiwa haki zote za kiraia bila ya kubaguliwa. Kufanya vingine ni kukubali kuwa nchini huku kuna matabaka mawili ya uraia, walio wengi wasio wasenge au wasagaji na walio wachache walio “gay.”
Neno la mwisho ni hili: kutoa hoja kwamba misahafu kama vile Torati, Biblia, au Kurani kwa inasema mwenendo huo dhambi ni kukiuka katiba ya Marekani inayosema bayana kabisa kwamba hakuna dini rasmi ya serikali au nchi na kwamba uhuru wa kuabudu (au kutoabudu) dini yoyote ni haki isiyopingika.
Suala la pili ambalo linatawala akili za wengi wa Tea Party ni kodi. Hawapendi kodi. Walakini iwapo kodi ni kitu cha lazima, basi ziwe ndogo sana, hasa kwa sekta ya biashara na watu walio matajiri. Tukipiga darubini msimamo huu tutagundua kuwa serikali si kama kampuni. Haina bidhaa za kuuza wala haina hudumu za kutoa kwa malipo. Njia kuu kwa serikali ya kidemokrasia ya  kujipatia pesa za kuendelezea nchi ni kwa kukusanya kodi kutoka kwa wananchi wote, maskini kwa matajiri, pamoja na makampuni na mashirika. Pasipo kodi serikali itawezaje kuboresha miundo mbinu ya nchi ili kufanya ukarabati madarajani, mabarabarani, n.k? Itawezaje kujenga mashule au kuinua hali ya elimu nchini? Itawezaje kulipa mishahara ya askari polisi, wazima moto, wanajeshi, walimu, na watumishi wa serikali? Bila kodi, au kodi za kutosha, nchi ingesambaratika katika hali ya vurugu tupu.

Ubaguzi wa rangi ungali upo kwenye jamii ya Kimarekani hivyo lazima wengi kama si wote wa wana-Tea Party ni wabaguzi wa rangi, hata kama wako weusi wachache waliojiunga na vuguvugu hilo. Hili si jambo geni. Kihistoria na katika nchi zote kumekuwa na watu waliorubuniwa akili zao au waliojifikiria nafsi zao tu. Mathalan, enzi ya utumwa nchini huku kulikuwa na watumwa wengi waliowasaliti watumwa wenzao kwa kufichua mipango ya kutoroka ya watumwa wengine.

Na kuhusu suala la mgombea wa chama cha demokrat katika nafasi ya useneta huko South Carolina Mark Green ambaye ametokea kushinda kiajabu nafasi ya kuwa mgombea wa chama hicho jimboni humo nini mtazamo wa Profesa John Mtembezi?

Juu ya Mark Green sijui mengi kuhusu maisha yake na siasa zake. Nimesikia kuwa amekuwa na matatizo fulani na polisi na kwamba kabla ya kugombea ubunge wa South Carolina hali yake ya kiuchumi haikuwa nzuri. Sasa watu wajiuliza aliwezaje kupata 10,000 pesa za kimarekani kujiandikisha apate kugombea uchaguzi huo. Na pesa za kuendeleza kampeni yake nazo zikatoka wapi? Nimewahi kumsikia akiongea kwenye mahojiano ya redio na yeye si mbumbumbu, akili anazo za kutosha. Lakini bado yapo maswali na tuhuma juu yake. Chama cha Democrats hakimwungi mkono kikamilifu kikiamini kwamba yeye hawakilishi maslahi ya Mademocrats bali amekula njama na chama cha upinzani. Mademocrats wengi waamini Richard Green akiwa mgombea anayewakilisha chama chao kugombea kiti cha ubunge mwezi wa 11, atashindwa kwa urahisi na mgombea wa chama cha Republican.

NO COMMENTS