Je Miami Heat wamegeuka kuwa Miami Cold?

0
445

Lebron James mambo bado huko Miami.
Kocha wa Miami Heat Erick Spoelstra.

Timu ya mpira wa kikapu ya Miami Heat ya huko Florida hapa Marekani imejikuta ikiwa na kibarua kigumu cha kujipanga upya baada ya kushindwa kuonyesha makeke yeyote katika michuano ya awali ya ligi ya mpira wa kikapu hapa Marekani.

Timu hii ambayo ilianza kwa kusaini wachezaji wawili mashuhuri wa kutisha kwenye ligi ya NBA Lebron “King James” na Chris Bosh ambao walitangazwa kuungana na mkongwe wa Miami Duane Wade wakitajwa kuwa ndio mihimili mipya ya timu hiyo.

Lebron James alitumia muda wake wa kutangaza kuhama kwa mbwembwe nyingi na kulipiwa muda maalum na Televisheni ya ESPN ili kutangaza ni timu gani anayokwenda kujiunga nayo na baada ya kuchukua muda wake na  kutangaza na kuwaacha hoi wapenzi wake wa Cleveland Ohio na Marekani kwa ujumla, Lebron alieleza bayana kuwa lengo lake kwenda Miami si fedha ila lilikuwa ni uwezekano wa kupata pete yaani ubingwa akiwa na wachezaji wenzake mashuhuri.

Lakini siku za karibuni zimeonyesha kwamba safari ya Miami kuelekea kwenye ubingwa bado ni ndefu sana baada ya kufungwa mfululizo na Memphis Grizzlies na Indiana, mechi ambazo hawakutarajiwa kupoteza kazi iliyopo mbele yao ni kubwa na hivi karibuni mkutano wa wachezaji peke yao bila kumhusisha kocha ili kuangalia upya hali yao, si hivyo tu Lebron alionyesha wazi wazi kutoelewana na kocha wake Erick Spoelstra .

Lebron alionyesha wazi kumgonga bega kocha wake wakati wa mechi yao waliyopoteza dhidi ya Dallas wakati wa mapumziko na haikuwa kumgonga kwa bahati mbaya. Jumanne Novemba 30 Lebron alifanya kikao na Kocha wake huyo kwa muda wa nusu saa nzima ambapo baada ya kikao hicho kocha huyo alisema hilo ni suala zuri kwa timu yao ambayo inajaribu kumaliza kiini cha tatizo kwenye kambi yao kushindwa kupata ushindi hasa safu yao ya ushambuliaji.

Na hatimaye katika mchezo wa Jumatatu Novemba 29 walipata ushindi dhidi ya Washington Wizards 105-94 lakini James alikataa kusema kwamba kocha huyo alimtaka abadili mchezo wake msimu huu na kukataa kueleza ya kuwa kuna msuguano kati yao na kusema kuwa ndiye kocha waliye naye na anamuunga mkono kwa kila jambo na kukana kwamba alimgonga kwa makusudi bega walipopoteza mchezo wao dhidi ya Dallas.

NO COMMENTS