Je Al Shabab wataweza kumalizwa?

0
804
Kundi la Alshabab
Kundi la Alshabab

Kitisho cha kundi la wanamgambo la Somalia Al Shabab chenye mahusiano na Al qaeda kimethibitika kuwa si mchezo na huenda kikaleta utata mzito katika ukanda wa Mashariki wa Afrika.

Tayari kundi hilo limeshapeleka vitisho mbali mbali katika nchi za maeneo hayo kikiwaonya wasithubutu kushiriki katika jeshi la kulinda amani huko Somalia kwa kulipua mabomu mawili mfululizo katika jiji la Kampala siku ya fainali ya kombe la dunia.

Kundi hilo limetoa vitisho kadhaa na hatimaye Umoja wa Afrika umeamua kwa kauli moja kuwa wanajeshi wake wataweza kushambulia wale wa Al Shabab ikiwa watagundua kundi hilo linataka kufanya mashambulizi. Hayo ni mabadiliko makubwa kwani awali askari hao walikuwa wanaruhusiwa tu kujitetea ikiwa watakuwa hatarini na sio kufanya mashambulizi.

Serikali ya Marekani hivi karibuni kupitia mwanasheria wake mkuu Eric Holder aliyekwenda Uganda kumwakilisha Rais Obama kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) imesema iko tayari kuisaidia Afrika kwa vifaa na silaha na utaalam kupambana na waasi hawa hatari wa Al Shabab. Lakini ni wazi kuwa Marekani haitokaa ipeleke majeshi Somalia na ndio maana Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda alitoa ushauri wa wazi na kauli ya kijasiri kwamba Afrika lazima iamke na kupeleka majeshi kusaidia serikali ya Somalia.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona wazi hilo halitawezekana kwani nchi za Afrika zina matakwa tofauti na hali kila moja akiangalia ustaarabu wake ukiachilia mbali hali mbaya ya uchumi inayogonga nchi nyingi za Afrika, mpaka sasa ni Guinea pekee iliyotangaza kuongeza majeshi huko Somalia ambako tayari Uganda na Burundi wanayo majeshi yao.

Na kama mjuavyo Alshabab tayari wameshatoa onyo kwa nchi zipelekazo majeshi huko walipoanza kwa kuwalipua wananchi wa Uganda, lakini ni wazi nchi za Afrika inabidi ziamke na kuacha kutegemea misaada ya Marekani na nchi za Ulaya hasa inapokuja kwenye suala nyeti la usalama.

Nchi jirani ya Kenya tayari imeshatangaza kujiweka katika hadhari na kuwaangalia kwa makini raia wa Somalia nchini humo ambao wanasemekana wananunua  nyumba za fahari  kama karanga huku wakilipa fedha taslim na tena ni dola wala si fedha za nchini humo.

Kwa kiasi fulani hawa jamaa wanahusishwa na biashara haramu ya uharamia maana kwa nchi isiyo na mapato rasmi wananchi wake, fedha hizo wanazipata wapi au kwa kufanya biashara gani? na hawa wanajeshi wa kundi la Alshabab vifaa na silaha za kuwawezesha kupambana kila siku wanazitoa wapi? na fedha za kujikimu je? kazi ipo viongozi  Afrika kaeni macho.

NO COMMENTS