0
510
Obama akiwa makao makuu ya jeshi Pentagon
Obama akiwa makao makuu ya jeshi Pentagon

Rais Barack Obama wa Marekani ameweka shada la maua katika wizara ya ulinzi Pentagon nje kidogo ya jiji la washington Dc Jumamosi kwa ajili ya kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao kwenye mashambulizi ya kigaidi  ya ndege Septemba 2001.

Akihutubia waliohudhuria hafla hiyo huko Pentagon Jumamosi Bw.Obama alisema wale waliovamia Marekani siku ile sio tu walivamia majengo lakini pia Marekani yenyewe akiongeza kwamba heshima kubwa ambayo Marekani inaweza kuwapa wale waliokufa ni kuishi maisha yao kama wamarekani.

Mwenyekiti wa makamanda wa majeshi ya Marekani Admirali Mike Mullen alisema walionusurika na shambulizi la kigaidi la Pentagon wamewatunukia waliokufa  maisha yao ikiwa  ni pamoja  na kujitolea kwa jeshi katika vita tangu mashambulizi ya 2001.

Mapema Jumamosi Makamu wa Rais Joe Biden na viongozi wengine na raia wa kawaida walikusanyika katika mji wa New York katika ibada ya kumbukumbu kwenye uwanja wa Ground Zero eneo ambalo majengo pacha ya biashara World Trade Center yalibomolewa na mashambulizi ya kigaidi miaka 9 iliyopita.

Taliban inatumia maadhimisho ya mashambulizi ya Septemba 11 kusema kuwa Marekani inatakiwa kuondoka Afghanistan ikiongeza kuwa Marekani imepoteza nafasi yeyote ya kuimarisha amani na  taarifa iliyotolewa Jumamosi na Taliban  imekosoa kile Taliban walichokiita ni “sera mbaya za Marekani”  na kuonya kuwa juhudi za kivita za Marekani zinaweka wamarekani katika hatari kote nchini humo na duniani kwa ujumla.

Ujumbe wa Taliban uliotiwa saini na umoja wa Waislam huko Afghanistan pia ulisema kuwepo kinyume cha sheria kwa Marekani nchini humo kumepingwa na ilisema chaguo lililobaki kwa maafisa wa Marekani ni kuondoa majeshi yao yote nchini humo. – Habari kwa niaba ya Sauti ya Amerika  VOA.

SHARE
Previous articleIDD MUBARAK
Next articleLADY GAGA ATOA MPYA

NO COMMENTS