Archive for July, 2012
Clinton kufanya ziara Afrika
Posted in Uncategorized on July 31, 2012 by sunday Shomari
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton anaanza ziara ya Afrika Jumanne, Senegal ikiwa nchi ya kwanza katika ziara yake ya siku 10 barani humo ambayo pia itamfikisha Kenya na Uganda ili kuhamasisha maendeleo ya ukuaji uchumi na demokrasia.
Kwa mujibu wa VOA wizara ya mambo ya nje ya Marekani inasema Clinton atakutana Jumatano na rais mpya wa Senegal Macky Sall na kuonyesha nchi hiyo kama mfano wa uvumilivu wa taasisi za kidemokrasia.
Bw.Sall alimshinda rais wa zamani Abdoulaye Wade katika uchaguzi wa Machi baada ya mabishano kuhusu Bw.Wade kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Clinton atatembelea pia Sudan Kusini ikiwa ni taifa jipya la Afrika kufuatia kujitenga kwake na Sudan mwaka jana. Ziara yake inaingiliana na mdahalo wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa juu ya hatua zinazoweza kuchukuliwa kumaliza mzozo unaoendelea wa mafuta, uraia na mipaka kati ya nchi hizo mbili.
Clinton anatarajiwa kuelezea miradi ya Marekani juu ya HIV/UKIMWI, elimu na maendeleo wakati wa ziara yake. Nchi nyingine atakazotembelea Waziri Clinton ni pamoja na Malawi na Afrika Kusini.
Waziri Clinton amefanya safari kadhaa siku za nyuma Afrika kusini mwa jangwa la Sahara . Mwaka jana alitembelea Ethiopia, Zimbabwe na Tanzania.
WALIMU WAGOMA, WANAFUNZI NAO WACHACHAMAA, SERIKALI YAONYA, YATISHIA KUWAFUTIA MISHAHARA
Posted in Uncategorized on July 31, 2012 by sunday Shomari
Nchi imetikiswa. Mgomo wa walimu ulioanza jana katika sehemu mbalimbali nchini, umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu huku kukiwa na taarifa za matukio yasiyokuwa ya kawaida yaliyoambatana na mgomo huo usio na ukomo.
Katika sehemu mbalimbali nchini, walimu waliripotiwa kugoma kwa kutoingia madarasani na wengine walifika kazini na kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka hali iliyosababisha wanafunzi kurandaranda ovyo katika sehemu za miji iliyo karibu na shule hizo.
Mjini Dodoma ,wabunge jana walimbana Naibu Spika, Job Ndugai wakitaka shughuli za Bunge zisitishwe ili kujadili mgomo wa walimu ambao umeanza rasmi jana nchi nzima, na kuziacha shule nyingi zikiwa na walimu wakuu na wakuu wa shule pekee.Kusom zaidi bofya Read more »
Sakata ya Ulimboka :Bunge latikisika
Posted in Uncategorized on July 31, 2012 by sunday ShomariSakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven Ulimboka, limeibuka upya bungeni baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kuitaka Serikali itoe majibu ya kina kuhusu watendaji wake kutajwa kuhusikana na tukio hilo.
Kambi hiyo pia imeitaka Serikali ieleze sababu za watendaji hao kutokamatwa hadu sasa na kuhojiwa na vyombo vya dola, wakati kuna taarifa kuwa wanafahamika.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katia mwaka wa fedha wa 2012/13, Conchesta Rwamlaza alisema, haiwezekani Serikali kuendelea kukaa kimya wakati watendaji wake wanatajwa kuhusika katika tukio hilo.
Rwamlaza alikuwa akizungumza kwa niaba ya msemaji wa kambi hiyo, Dk Antony Mbassa, ambaye alitaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu kubaini ukweli.Kusoma zaidi bofya Read more »
Zitto ahojiwa kwa rushwa
Posted in Uncategorized on July 31, 2012 by sunday Shomari
Sakata la wabunge kuhusishwa na rushwa limeingia sura mpya, baada ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe kuhojiwa na chama chake cha Chadema kwa saa tatu jana.
Wakati Zitto akihojiwa, kambi rasmi ya upinzani bungeni, iliwataja wabunge saba wa CCM na kueleza kuwa ndiyo wanaolichafua Bunge kwa kujihusisha na mambo yenye maslahi binafsi wakiwa watumishi wa umma.
Kadhalika, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) ilikuwa ikiendelea kuwahoji baadhi ya wabunge kuhusu tuhuma za rushwa na kwamba uchunguzi ukikamilika taarifa zitawekwa wazi.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, jana aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Tweeter kwamba alihojiwa na Sekretarieti ya chama chake kutokana na tuhuma za rushwa zinazowagusa badhi ya wabunge.
Katika maelezo yake, Zitto alisema aliiambia sekretarieti ya chama hicho kwamba Chadema kifanye uchunguzi ili kubaini ukweli wa suala hilo na kwamba yuko tayari kuwajibika ikiwa itathibitika kwamba alihusika kula rushwa.Kusoma zaidi bofya Read more »
CCM,Chadema wawatangazia kiama wabunge mafisadi
Posted in Uncategorized on July 30, 2012 by sunday Shomari
Vyama vya CCM na Chadema vimetoa onyo kali kwa wabunge wanaotuhumiwa kwa kashfa ya kuhongwa na baadhi ya kampuni za mafuta na kulihujumu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), vikisema havitasita kuwawajibisha pindi tuhuma hizo zitakapothibitika.
Kauli ya vyama hivyo imekuja siku moja baada ya wabunge watano, watatu wa CCM na wawili wa upinzani kudaiwa kuhusika na vitendo hivyo vya rushwa, ambavyo vimesababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili majina ya wahusika yawekwe hadharani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa juu wa vyama hivyo walisema wanasubiri kwa hamu taarifa rasmi kutoka bungeni.Kusoma zaidi bofya Read more »
Wabunge wazidi kuongezewa marupurupu
Posted in Uncategorized on July 30, 2012 by sunday ShomariMarupurupu ya wabunge ikiwamo mishahara imeongezwa kutoka Sh7.4 milioni kwa mwezi hadi takriban Sh11milioni kwa mwezi, hatua ambayo imeibua mjadala mwingine mzito miongoni mwao.
Tangu mwaka jana, wabunge wamekuwa katika vita ya kupokea au kutopokea posho ya vikao ambayo imekuwa ikikolezwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ambaye alizikataa akisema mbunge anapokuwa kazini hahitaji kulipwa.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba sasa vita kubwa ipo katika marupurupu mapya ambayo pamoja na kuchanganya na mshahara yanafikia Sh11milioni kwa mwezi.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alipoulizwa jana alithibitisha kuhusu kuongezeka kwa malipo jumla ya wabunge kwa mwezi lakini akasema hafahamu kiwango halisi kilichoongezwa.Kusoma zaidi bofya Read more »
Museveni atoa tahadhari ya Ebola
Posted in Uncategorized on July 30, 2012 by sunday Shomari
Rais wa Uganda ametahadharisha wananchi wa Uganda dhidi kugusana gusana baada ya muathirika wa kirusi kikali cha homa ya Ebola kuripotiwa katika mji mkuu Kampala.
“Wizara ya afya inawasiliana na watu wote waliokutana na mgonjwa huyo,” alisema Rais Museveni katika hotuba ya taifa akiongeza kuwa watu 14 wamefariki tangu homa ya Ebola kulipuka magharibi mwa nchi wiki tatu zilizopita.
Wagonjwa wawili wameripotiwa Kampala, mmoja akafariki katika hospitali kubwa ya Mulago. Rais ametaka watu wasishikane mikono wanaposalimiana kuepuka kueneza ugonjwa huo.
Madakatari saba na wafanyakazi wengine wa afya 13 katika hospitali ya Mulago wapo katika karantini baada ya wagonjwa “mmoja au wawili” kupelekwa katika hospitali hiyo.





