Nchi ya Pakistan imekumbwa na mafuriko mabaya kuliko yote katika historia ya nchi hiyo kwa mujibu wa Umoja wa mataifa mafuriko hayo yameleta maafa makubwa kuliko tsunami kwenye bahari ya Hindi 2004, tetemeko la Kashmir 2005 na tetemeko la Haiti 2010 kwa pamoja.
Lakini wachambuzi wanaeleza ni kwa nini pengine inafikiriwa kama vile mafuriko haya si makubwa kama ilivyokuwa majanga haya mengine na wameeleza kuwa ni kutokana na idadi ya watu waliokufa kuwa ni ndogo kuliko hayo majanga mengine.
Lakini kwa mujibu wa Umoja wa mataifa mafuriko haya ni makubwa sana kwasababu mpaka sasa idadi ya walioathirika ni kubwa mno na inaripotiwa kuwa wanawake wajawazito pekee ni laki 5 ambao hawana makazi mpaka sasa na karibu watu milioni 13 kwa jumla hawana mahali pa kuishi. Idadi ya vifo inakadiriwa kuwa 1500 mpaka sasa.
Watu wengi wanalala kwenye miti na mahema na wamegeuka wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe. Nchi hii inahitaji msaada mkubwa kwa kweli. Mpaka sasa Marekani imeahidi kutoa dola milioni 150 kusaidia nchi hiyo, lakini hali ya misaada bado inasemekana ni ndogo sana na inapatikana kwa taratibu sana kwani inachukua muda mrefu kuwafikia walengwa.




